Thursday, 3 November 2016

RPC KINONDONI ATOA TAHADHARI KWA WAMILIKI WA MAGARI JIJINI DAR ES SALAAM

RPC Suzan Kaganda

Na Dotto Mwaibale

WAMILIKI wa magari wametakiwa kuchukua tahadhari ya kuzima na kufunga milango magari yao pale wanaposimama kwa dharura kupata mahitaji mbalimbali ili kuyanusuru kuibwa.

Mwito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Suzan Kaganda wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu tukio la kuibwa kwa gari la Kapteni Innocent Dallu maeneo ya Mbezi Juu huku akiwemo mtoto wake Lightness.
"Napenda kutumia fursa hii kuwaomba wamiliki wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari ya kuzima magari yao na kufunga milango wanaposimama maeneo yoyote kupata mahitaji yao kwani si rahisi kumbaini mhalifu kwani wapo kila sehemu" alisema Kaganda.

Alisema katika tukio la kuibwa kwa gari la kampteni Dallu alikuwa amesimama maeneo ya Mbezi Juu bila ya kulizima akinunua mahitaji ambapo walitokea vijana wakaondoka na gari hilo aina ya Toyota Harrier baada ya kumtelemsha mmoja wa watoto aliyekuwemo ndani ya gari hilo aitwaye Philip huku wakiondoka na mdogo wake Lightness.

Alisema watuhumiwa hao walimtelekeza mtoto huyo maeneo ya Golden Bridge katika baa moja na kisha kuondoka na gari hilo ambalo lilipatikana baada kukamatwa na polisi Kiwangwa mkoani Pwani ambapo  kijana mmoja Ezekiel Daud anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.

Alisema ni vizuri wamiliki wa magari kuzingatia jambo hilo ili kuepusha matukio kama hayo ambayo yanapoteza muda mwingi wa kuyatafuta kwani tukio kama hilo lilitokea hivi karibuni maeneo ya Kinondoni ambapo wahalifu waliweza kuiba gari aina ya Noah lililosimamishwa bila ya kuzimwa na kuondoka nalo na alijapatikana mpaka leo hii.

No comments:

Post a Comment