Thursday, 3 November 2016

SERUKAMBA: TUMEKAMILISHA KAZI MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI


Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imemaliza kazi yake ya kupitia maoni yailiyowasilishwa na wadau, taasisi na wananchi ili kuboresha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari nchini ambao unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili Bungeni hivi karibuni.
Akifanya majumuisho ya mjadala wa kuchambua maoni yaliyowasilishwa, Mwenyekiti Kamati hiyo Peter Serukamba - pichani juu - amesema kuwa wameyapitia maoni yaliyowasilishwa kifungu kwa kifungu na kuna maeneo ambayo Serikali wameyapokea na kamati inaendelea kuyafanyia kazi.

Serukamba amesema kuwa Muswada huo ni miongoni mwa miswada ambayo imekuwa unajadiliwa kila mara na watu mbalimbali nchini na kamati yake imeufanyia kazi Muswada huo kwa kuboresha baadhi ya maeneo.

“Katika miswada ambayo wananchi wameisoma na kusikilizwa sana ni Muswada huu, maana ndio Muswada pekee ambao kwa kweli umejadiliwa sana katika vyombo vya habari; kwenye magazeti, kwenye radio na Tv kupitia vipindi maalum vya kujadili Muswada huu na maoni yao mengi yameingizwa kwenye Muswada huu” alisema Serukamba.

Serukamba ameyataja maeneo ambayo Kamati yake imefanyia kazi na kuyaingiza kwenye Muswada kama maboresho kulingana na maoni yaliyowasilishwa ni pamoja na namna ya kumtambua mwandishi wa habari, namna ya kulinda haki za waandishi wa habari, kulinda haki za wenye vyombo vya habari pamoja na kumlinda mtu yeyote katika jamii.

Katika kulinda haki za mtu yeyote kutokana na kutendewa ndivyo sivyo kupitia vyombo vya habari ikiwamo watu kutukanwa ambapo awali kesi hizo zilikuwa zinachukua muda mrefu, Serukamba amesema kuwa Muswada huo umeweka utaratibu ambao unafanya kesi inapofunguliwa iweze kuendeshwa kwa muda mfupi kadiri inavyowezekana ili mtu apate haki zake.

Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa wananchi na wadau wengi wametoa maoni yao ya kuboresha Muswada kwa njia mbalimbali kwa kuwa walikuwa wanaongea na Kamati kupitia vyombo vya habari na wengine wameandika na kamati imeyafanyia kazi.

“Mimi na wanakamati wenzangu tunajivunia kwamba tumeandika historia hii ambayo iliwashinda wengine wote tangu mwaka 1993, sisi tumeweza kuleta Sheria nzuri ambayo itasaidia waandishi wa habari, itasaidia tasnia ya habari Tanzania na tutaanza kuwajibika kama taifa na ni mwanzo mpya kwa uandishi wa habari Tanzania” alisema Serukamba.

Serukamba amewatoa hofu wadau wa habari juu ya kuanzishwa kwa Sheria hiyo kwa kuwaasa kuusoma muswada huo ambao utaifanya tasnia ya habari kwa taaluma na pia sheria imetoa muda wa mpito wa miaka mitano pamoja na kuanzisha Baraza Huru la Habari pamoja na kusimamia maslahi ya waandishi wa habari nchini. 

Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Kamati Serukamba amevipongeza vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya Muswada huo kwa kuwa na mijadala ambayo imekuwa ndio jukwaa lililosaidia kuwaelimisha wananchi juu Muswada wa Huduma za Habari kwa kuwa kamati yake imepata maoni mengi kupitia mijadala iliyoendeshwa kwenye vyombo vya habari.

No comments:

Post a Comment